Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA – Maelfu ya waumini na wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) jana Jumapili walijitokeza kwa wingi katika Wilaya ya Temeke, jijini Dar -es- Salaam, kushiriki Masira ya A'shura yaliyofanyika kwa lengo la kuhuisha Mapinduzi ya Imam Hussein bin Ali (as) na kukumbuka tukio la kusikitisha la Karbala.
Washiriki wa matembezi hayo walilaani mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saww), Imam Hussein (as), pamoja na familia yake na masahaba wake waliouawa na jeshi la Yazid bin Muawia katika ardhi ya Karbala mwaka 61 Hijria.
Katika ujumbe wao, waumini hao walisisitiza kuwa Masira ya A'shura ni ishara ya kuendeleza malengo ya Imam Hussein (as) ya kuulinda na kuuhuisha Uislamu wa asili na halisi wa Mtume Muhammad (saww), kupinga dhulma, ufisadi na batili, na kusimama imara katika kutetea haki, uadilifu na heshima ya mwanadamu.
Washiriki wa Masira hayo pia walibeba mabango yenye ujumbe wa amani, umoja na mapambano dhidi ya kila aina ya dhulma, wakisisitiza kuwa ujumbe wa Karbala unaendelea kuwa nuru na mwongozo kwa Waislamu na watu wote wanaopigania haki duniani.
Viongozi wa dini walioshiriki katika tukio hilo walieleza kuwa kumbukumbu ya A'shura si tukio la kihistoria pekee, bali ni shule ya maadili na mapinduzi inayowafundisha watu kusimama dhidi ya dhulma, kutetea wanyonge na kujitoa kwa ajili ya kulinda haki na misingi ya dini.
Masira ya A'shura hufanyika kila mwaka katika maeneo mbalimbali duniani kama sehemu ya kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (as) na ni fursa ya kuhuisha maadili ya kujitolea, kusimama dhidi ya dhulma na kutetea misingi ya dini na utu wa mwanadamu.
Your Comment